Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), ameendelea kuweka pingamizi dhidi
ya Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam Tanzania, Sheikh Issa Ponda
akipinga maombi yake ya kufanya marejeo ya uamuzi wa Mahakama ya Hakimu
Mkazi Morogoro.
Sheikh Ponda anakabiliwa na kesi ya jinai katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, akidaiwa kufanya uchochezi maeneo
mbalimbali mkoani humo na kukaidi amri ya Mahakama ya Kisutu ya Mei 9,
mwaka jana ya kumtaka kuhubiri amani kwa jamii likiwa ni sharti la
kifungo cha mwaka mmoja nje.
Awali, Sheikh Ponda aliomba Mahakama ya Hakimu
Mkazi Morogoro imfutie shtaka hilo la kukaidi amri ya Mahakama ya
Kisutu, lakini Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro ilimkatalia, aliamua
kuwasilisha maombi Mahakama Kuu akiiomba ifanye marejeo ya uamuzi huo.
Hata hivyo, maombi hayo yalitupiliwa mbali Desemba
11, mwaka jana baada ya DPP kumwekea pingamizi kuwa hati ya kiapo
iliyokuwa ikiunga mkono maombi yake, ilikuwa na kasoro za kisheria kwa
kuwa haikuwa ikitimiza matakwa ya Sheria ya Viapo kwa kutokuonyesha jina
la aliyeapa na tarehe.
Baada ya kutupiliwa mbali, Wakili wa Ponda, Juma Nassoro aliwasilisha tena maombi hayo.
mahakamani hapo baaada ya kufanya marekebisho ya kasoro hizo za kisheria.
Maombi hayo mapya yalipangwa kusikilizwa jana na
Jaji Augustine Mwarija, lakini yalikwama baada ya DPP kuwasilisha tena
pingamizi la awali akiiomba mahakama iyatupilie mbali akidai kuwa
yamewasilishwa kinyume na kifungu cha 372 (2) Sheria ya Mwenendo wa
Makosa ya Jinai (CPA).
No comments:
Post a Comment