WATU
wasiofahamika majina wala makazi yao, juzi walifunga Barabara Kuu ya
Mbeya-Njombe, Wilaya ya Mbarali, mkoani Mbeya kwa kuweka mawe, magogo,
kuteka magari na kujeruhi abiria waliokuwa katika magari hayo.
Akizungumza
na waandishi wa habari mjini Mbeya jana, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani
humo, Robert Mayala, alisema tukio hilo lilitokea saa 1:30 usiku,
Kijiji cha Machimbo, Kata ya Rujewa.
Alisema
watu hao walikuwa na silaha za jadi kama mapanga, rungu, mawe na fimbo
ambapo katika tukio hilo, baadhi ya abiria walijeruhiwa na kuporwa vitu
mbalimbali.
Vitu hivyo ni pamoja na pesa taslimu, simu za mkononi na mikoba ambayo thamani yake wala idadi haijafahamika.
"Hawa
watu waliwashambulia baadhi ya abiria kwa kuwapiga sehemu mbalimbali za
miili yao kwa kutumia silaha ambazo walikuwa nazo, kufanya uharibifu
katika baadhi ya magari kwa kuvunja vioo," alisema Kamanda Mayala.
Aliongeza
kuwa, katika tukio hilo Bw. Mashaka Abdallah ambaye ni dereva,
alijeruhiwa vibaya na kulazwa Hospitali ya Serikali wilayani Mbarali na
hali yake inaendelea vizuri; watu wengine wawili walipatiwa matibabu na
kuruhusiwa.
Alisema
polisi waliokuwa doria eneo la Igawa, Mbeya na Njombe walifika eneo la
tukio na magari mengi yakiwemo yanayosafirishwa kwenda nje, yakiwa
yamesimamishwa.
"Watu
hao walipoona gari la polisi walikimbilia vichakani na magari hayo
yaliondoka chini ya ulinzi wa polisi kuendelea na safari, watu 10
tunawashikilia kwa mahojiano," alisema.
No comments:
Post a Comment