Serikali
imesema inatarajia kuwa kodi ya ving'amuzi itashuka ili kuhamasisha
kampuni nyingi zaidi kujitokeza kuuza vifaa hivyo kwa wananchi, tofauti
na sasa.
Hayo yalisemwa mjini hapa mwishoni mwa wiki na Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba, wakati akifunga
mkutano wa jukwaa la kujadili mchakato wa kuhama kutoka mfumo wa
analojia kwenda digitali, uliohusisha nchi zaidi ya 25 duniani.
"Bei za ving'amuzi ipo chini japo sisi serikali tunaona bado ipo haja
tupunguze kodi zaidi ili ishuke chini zaidi kwa ajili ya kuwezesha
makampuni mengi kununua vifaa hivyo na kuwauzia wananchi hasa waliopo
vijijini," alisema.
Aidha, Naibu Waziri huyo alisema ni nia ya serikali kuona vijana wengi
wanawezeshwa kwa kujikusanya kwenye vikundi vyenye uwezo wa kutengeneza
vipindi vya televisheni na makala ili waweze kujiingizia kipato.
Alisema kabla ya Tanzania kuingia katika mfumo wa dijitali, wamiliki
wengi wa televisheni ndiyo waliokuwa wanatengeneza vipindi na makala
mbalimbali kwenye vituo vyao, lakini kwa sasa baada ya mfumo huo
kuanzishwa kuna fursa ya vijana kutengeneza wenyewe vipindi hivyo.
"Kilichopo hapa vijana wajiendeleze ili wawe na ujuzi wa kutengeneza
makala na kuandaa vipindi ambavyo vitatumika kwenye vituo vya
televisheni na hatua hii itawawezesha kupata fedha za kutosha," alisema.
Alisema moja ya maazimio ya mkutano huo ni kuona bei za televisheni
zinashuka zaidi ili wananchi wengi wamudu kuzinunua kwa ajili ya
kujipatia habari za dunia zinazoendelea na masuala mengine mbalimbali.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA),
Profesa John Nkoma alisema mfumo wa dijitali umesaidia wananchi kwa
upande wa simu za viganjani kuwasiliana na mtu yoyote kwa njia
mbalimbali zilizoko kwenye simu hizo.
"Haya ni matunda ya dijitali na maendeleo yamekuwa makubwa sana katika
utumiaji wa simu hizi, kama vile wengi wanawasiliana kwa Wa-tsap, lakini
kwa upande wa televisheni ni ngumu kidogo kuingia maeneo yote kwa mara
moja," alisema.
Profesa Nkoma alisema awamu ya pili ya uzimaji wa mitambo ya analojia
itakuwa katika mikoa ya Morogoro, Tabora, Musoma, Mara na Dodoma na
ifikapo Juni 2015 nchi nzima itakuwa imeingia katika mfumo wa dijitali
kama makubaliano ya Geneva yanavyosema.
Kuhusu uvumi wa kwamba mfumo huo unauwa televisheni za zamani, alisema
ni kitu cha kupuuza kwani hakina ukweli, kwani kitu kinachotakiwa ni
kununua king'amuzi na mhusika ataendelea kupata matangazo ya
televisheni kama kawaida.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment