Serikali
mkoani Pwani imefuta vibali vya uendeshaji wa mabanda ya kuonyesha
video wilayani Kibaha pamoja na kuanzisha uchunguzi wa wanafunzi wa
shule msingi wanaojihusisha na vitendo vya ulawiti.
Hatua hiyo inachukuliwa baada ya wanafunzi wa kiume wa shule za
msingi wilayani humo kudaiwa kufanya vitendo hivyo vyenye athari kiafya
na kitaaluma.
Katika hatua nyingine, polisi wilayani humo inawashikilia watu
wawili waliokutwa wakiendesha biashara ya kuonyesha video chafu kwenye
mabanda kinyume na sheria.
Toleo la Nipashe la Jumapili iliyopita liliripoti taarifa za
wanafunzi katika shule tatu zilizopo Mlandizi, wilayani humo
wanaojihusisha na vitendo vya kujaamiana kinyume cha maumbile wenyewe
kwa wenyewe, pamoja na watu wengine kutoka nje ya shule hizo
wakiwadhalilisha kingono.
Taarifa za uhakika zilisema tayari timu maalum imeundwa na uongozi
wa mkoa huo kwa ajili ya kuchunguza suala hilo na wajumbe watatembelea
shule zilizotajwa katika mahojiano na wanafunzi pamoja na walimu.
Akizungumza na NIPASHE, Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kibaha, Amedeus
Marenge, alisema pamoja na kushikiliwa watuhumiwa hao wawili,
wamefungua jalada la uchunguzi katika shule mbalimbali wilayani humo
kubaini washukiwa.
Alisema wanaoshikiliwa siyo kwamba wanahusika moja kwa moja na
tuhuma hizo, bali mabanda wanayoyamiliki yanatumiwa kudhalilisha watoto
na kuonyesha picha zisizo na maadili.
"Kazi ya kuchunguza suala kama hili ni ngumu kwa sababu mambo yote
yanafanyika sirini na hakuna aliyejitokeza kusema ukweli. Uchunguzi
wetu unaendelea ….," Alisema Marenge.
Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya aliwataka wananchi hasa wazazi
kushirikiana na polisi kwa kutoa taarifa wanapoona mambo yanayowapa
mashaka kuhusu mienendo ya watoto wao.
HALMASHAURI YAFUTA VIBALI
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kibaha, Tatu Selemani, alisema kuanzia
sasa shughuli ya uonyeshaji video kwenye mabanda umepigwa marufuku.
Alisema amemuagiza Afisa Utamaduni kufuta vibali pamoja na kuwafuatilia wanaoonyesha picha hizo.
"Nimeagiza vibali vyote vifutwe na marufuku kwa kuendesha shughuli hiyo hata kama wana malengo ya kuonyesha soka,"alisema.
Uchunguzi wa gazeti hili uliofanywa maeneo hayo ulibaini mabanda mengi ya aina hiyo yamefungwa na kufuli.
WANANCHI WAPONGEZA
Baadhi ya wazazi waliipongeza serikali kuingilia kati na
kuwanusuru wanafunzi ambao walianza kupotoka na kuongeza kuwa kusitishwa
uonyeshaji wa picha za video kumewezesha watoto kuanza kwenda shuleni.
"Viongozi wa serikali walikuja hapa Jumatatu na kufunga vibanda
hivi jirani na shule za msingi Mtongani na Azimio, tumeanza kuona
matokeo mazuri kwani watoto wanakwenda shule na kuhudhuria vipindi ,"
alisema Hamisi Kondo mkazi wa Mtongani.
Mzazi mwingine Christopher Steven, aliwapongeza wanafunzi na
walimu walioibua suala hilo kwa kuowaokoa watoto wengi ambao wangeingia
katika mazingira hayo hatarishi.
"Unajua sisi wazazi tumekuwa na tabia ya kutosikiliza yanayosemwa
na walimu, badala yake tunasubiri hadi mambo yawe makubwa ndipo
tunashtuka, naamini wanafunzi na walimu wametupa mwanga na nia yao
ilikuwa kuokoa watoto wetu, tunashukuru," alisema Steven.
Uchunguzi huo ulioibua matukio hayo ulifanywa katika shule za
msingi za Mtongani, Azimio na Jamhuri zilizoko mji mdogo wa Mlandizi na
yaliyohusisha wanafunzi wa darasa la tatu na la nne ambao mara nyingi
wanalazimishwa kulawitiwa na wenzao wa madarasa ya juu.
Aidha ilidaiwa wanafunzi wengine wanafanyiwa vitendo hivyo na watu
wazima wakiwa majumbani kwao na kwenye mabanda yanayoonyesha picha za
video nyakati za usiku.
Ilielezwa kwamba ndani ya mabanda hayo watoto waliingiliwa na watu wazima baada ya kuangalia picha za ngono.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment