"Katiba yetu isiruhusu wachache wenye
nguvu ya kisiasa, kiuchumi na kiutawala kutumia vibaya uwezo wao na
kusababisha utengano kitabaka,"
Dodoma. Tume ya Haki na Amani ya
Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), imetoa tamko ikitaka Bunge Maalumu la
Katiba kuepuka kukashifu mapendekezo ya muundo wa Serikali tatu.
TEC imesema muundo wa Serikali mbili
haukutatua matatizo ya msingi na badala yake ulilimbikiza kero
zilizosababisha Zanzibarkujiundia Katiba yake mwaka 2010 bila
kushauriana na Tanzania Bara.
Tamko hilo limesainiwa na Mwenyekiti
wa tume hiyo, Askofu Mkuu, Paulo Ruzoka. Tume hiyo imesema pendekezo la
Serikali tatu litawarudisha Watanzania hali ya kuwa na umoja.
"Pendekezo la Serikali tatu
lililowekewa mazingira tekelezi yakitoa mwanya wa kuboresha muundo huo
kwa njia ya uwazi, shirikishi na za kidemokrasia lina tija kubwa ya
kuturudishia umoja," limesema.
Tamko hilo la kurasa 15 limetolewa
baada ya mkutano wa kitaifa wa wajumbe wa Kamati za Majimbo za Haki na
Amani za kanisa hilo na Chama cha Wanataaluma Wakatoliki Tanzania (CPT),
uliofanyika Februari 5 na 6 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
CPT ambayo imekuwa ikitumika kutoa
matamko ya Kanisa Katoliki nchini na kuibua mijadala mizito, imesambaza
tamko hilo kwa wajumbe wa Bunge la Katiba ambao ni marafiki wa chombo
hicho, ikiwaomba walitumie tamko hilo kutafakari wakati wakijiandaa na
mijadala katika Bunge hilo.
Tume hiyo ya TEC imesema baada ya
kuchambua Rasimu ya Pili ya Katiba, wajumbe wa mkutano huo waliridhia
kuwa Katiba inayoandaliwa si ya wanasiasa, vyama vya siasa wala asasi za
kidini.
"Katiba yetu isiruhusu wachache wenye
nguvu ya kisiasa, kiuchumi na kiutawala kutumia vibaya uwezo wao na
kusababisha utengano kitabaka," limesisitiza tamko hilo.
Tamko hilo limesema pendekezo la
muundo wa Muungano wa Serikali tatu si jambo kuu kuliko mengine yote
katika rasimu hiyo na kusisitiza kuwa Bunge lisikashifu mapendekezo
hayo.
"Rasimu ya pili ni hatua njema katika
tukio muhimu na la kihistoria nchini Tanzania. Tunatarajia Bunge Maalumu
lisimkane Mungu na lisikashifu mapendekezo ya Serikali tatu," limesema.
Kanisa hilo limesema duniani hakuna
Katiba yoyote kamilifu na kwamba Watanzania waanze na rasimu
iliyopendekezwa na Katiba hiyo iendelee kuboreshwa pale itakapobidi.
"Tunawaalika wananchi wote wa Tanzania
kwa dhamira moja, kuliombea na kulisaidia Bunge Maalumu la Katiba
liweze kufanya kazi yake kwa ustadi na kujali masilahi ya taifa,"
limesema tamko hilo.
Tamko hilo limekuja wakati Bunge la Katiba likiwa njia panda kutokana na wajumbe wake kuyumbishwa na misimamo ya vyama.
Wajumbe hao wameshindwa kuafikiana
kuhusu namna ya kupiga kura wakati wa kupitisha vifungu vya Katiba, huku
CCM ikishikilia msimamo wa kutaka kura ya wazi na makundi mengine kura
ya siri.
Kabla ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2010,
taasisi hiyo ya kidini ilitoa matamko mawili, moja juu ya sifa za
viongozi wanaostahili kuchaguliwa na jingine la ilani ya uchaguzi ya
kanisa hilo, mambo ambayo yaliibua mijadala mizito.
Chanzo, mwananchi
No comments:
Post a Comment