Jeshi la Polisi linamshikilia dereva mmoja wa pikipiki, maarufu kama bodaboda wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro baada ya mke wa askari polisi kukutwa amekufa chumbani kwa dereva huyo.
Tukio hilo ambalo limezua gumzo kubwa wilayani
humo lilitokea juzi saa 12:00 jioni katika eneo la New Mwanga wilayani
humo na mtuhumiwa akidaiwa kukutwa akiwa amelewa chakari.
Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Shaibu Ndemanga amethibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kusema uchunguzi unaendelea.
“Hilo tukio lina ukweli na bahati mbaya sana
mumewe ndiyo kwanza amehamishiwa Geita na alikuwa akaripoti halafu aje
kuchukua familia yake,” alisema Ndemanga.
Mkuu huyo wa wilaya ambaye pia ni mwenyekiti wa
kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo, alisema hadi sasa
haijafahamika nini kilitokea na kwamba hilo ni moja kati ya mambo ambayo
polisi inachunguza.
“Hayo yote kwamba ilikuwaje akawa chumbani kwa
huyo kijana, nini sababu za kifo yatajulikana kadiri upelelezi
unavyoendelea,” alisema.
Imeelezwa kuwa jana ilikuwa siku ya askari huyo kuripoti katika kituo chake kipya cha kazi.
“Mpaka sasa hivi haijajulikana nini hasa kilitokea
huko chumbani na ilikuwaje akawa chumbani kwa huyo dereva,” alisema
mmoja wa watu waliokuwapo katika eneo la tukio ambaye hata hivyo,
hakutaka kutaja jina lake na kuongeza kuwa jana saa sita mchana, mwili
wa mwanamke huyo ulichukuliwa kutoka Hospitali ya Wilaya ya Mwanga na
kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC kwa uchunguzi.
Taarifa za awali zinasema kuwa mwili wa marehemu ulikuwa na mikwaruzo shingoni hali inayotia shaka kuwa huenda alinyongwa.
Habari nyingine zinadai kuwa siku ya tukio,
mwanamke huyo alikuwa ameaga kuwa anakwenda kanisani lakini baadaye simu
yake ilipopigwa ilikuwa ikipokewa na mwanamume.
Ilidaiwa kuwa mume wa marehemu alipojaribu kupiga
simu ya mkewe, ilikuwa ikipokelewa na mtu aliyeonekana kuwa ni mlevi wa
kupindukia hali iliyomtia wasiwasi na kuamua kuwapigia simu marafiki
zake wa karibu ili wamsaidie kumtafuta ndipo walipopata taarifa kuwa
ulikuwapo uhusiano kati ya shemeji yao na dereva huyo wa bodaboda.
Ilidaiwa kuwa marafiki hao walikwenda moja kwa
moja nyumbani kwa dereva huyo wa bodaboda ambako walimkuta akiwa amelewa
na walipoingia ndani walimkuta shemeji yao akiwa ameshafariki dunia.
Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Robert Boaz hakupatikana jana kuzungumzia tukio hilo kwa kuwa alikuwa kwenye ziara ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda huko Gonja wilayani Same.
Credit: Mwananchi
Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Robert Boaz hakupatikana jana kuzungumzia tukio hilo kwa kuwa alikuwa kwenye ziara ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda huko Gonja wilayani Same.
Credit: Mwananchi
No comments:
Post a Comment