Akizungumza kwenye mkutano huo wa
marekebisho ya Katiba ya Simba, Rage alisema: “Simba oyee…Wanasimba
msifanye makosa Mei 4 hakikisheni mnachagua kiongozi ambaye atakaa
madarakani miaka minne, msifanye makosa baada ya mwaka mmoja mkataka
aondoke, Katiba ya Simba inakataza mapinduzi.
“Mimi sitagombea, mimi siyo maskini, sina njaa, hata mkizomea nasemaje mimi sina njaa, na wanachama wengi mliopo hapa ni mambumbumbu.”
Kauli hiyo iliamsha hasira kwa baadhi
ya wanachama ambao walitaka kumvamia na kumtwanga makonde, lakini
Polisi waliingilia kati na kusababisha wanachama kupambana na wale
wanaomuunga mkono Rage, tafrani hiyo ilidumu kwa zaidi ya nusu saa hadi
pale Rage alipoomba radhi kwa kutangaza kuifuta kauli yake hali ikatulia
na mkutano ukaanza.
Hata hivyo mkutano huo ulifanyika
huku akidi ya wanachama ikiwa haijatimia kwani ili akidi itimie
ilitakiwa kuwe na wanachama 250 na kuendelea, lakini wanachama waliofika
jana ni 166 ambao hawafikii hata nusu ya akidi ya wanachama ambayo
inatambulika kwa mujibu wa Katiba ya Simba.
Katika mkutano huo wanachama
walipinga kuburuzwa kwa kuwepo kipengele cha ibara ya 11 (a) ambacho
kinakataza mwanachama kuzungumza na vyombo vya habari isipokuwa vikao
halali, na mwanachama atakayefanya hivyo tawi limuwajibishe ndani ya
siku 14 tangu kutokea kwa kitendo hicho, wanachama hao waligoma na
kutaka kifungu hicho kiondolewe kwani kinawaminya uhuru na haki ya
kuzungumza.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF,
Geofrey Nyange naye alijikuta akizodolewa na Rage pale aliponyoosha
kidole na kusema: “Taarifa mwenyekiti…taarifa, huku akisimama na
kujibiwa na Rage ‘Siyo lazima usimame, kaa chini, nimesema siyo lazima,
mwingine’ alisema Rage na kuteua mwanachama mwingine kuchangia hoja yake
kabla ya kumpa nafasi Kaburu.
Akichangia kuhusu kipengele hicho
Kaburu alisema: “Hakuna eneo ambalo TFF ilisema kuhusu kifungu hiki,
haya ni mawazo yetu ni kweli baadhi ya wanachama wanatukana viongozi
ndio maana kikawekwa ili kuminya wanachama wakorofi, kwa vile tupo hapa
kwa ajili ya kuunda Kamati ya Maadili wakorofi wote watapelekwa kamati
ya maadili ndio watawajibishwa huko siyo kuingiza kwenye katiba,”
alisema Kaburu na kushangiliwa na wanachama wengi.
Kipengele kingine ambacho kinasubiri
huruma ya TFF ambacho Simba wamekipitisha kwa kishindo ni kile cha ibara
ya 26 kinachozungumzia sifa za wagombea, fasili ya tano ya katiba ya
Simba ya zamani inasomeka: ‘Asiwe aliyewahi kutiwa hatiani kwa kosa la
jinai kwa kuhukumiwa kifungo’.
Wanachama hao wametaka kifungo hicho
kisomeke ‘Asiwe ametiwa hatiani kwa kifungo cha zaidi ya miezi sita bila
mbadala wa adhabu na endapo ametiwa hatiani kwa kifungo cha zaidi ya
miezi sita, awe amemaliza muda wa miaka mitano tangu kuisha kwa kifungo
husika bila kutiwa hatiani kwa kosa lingine lolote la jinai.
Kipengele hicho (b) kimeongezwa
maneno yanayosomeka: ‘Mgombea ni lazima awe ametimiza angalau mwaka
mmoja wa uanachama na si miaka mitano kama ilivyo sasa.’
No comments:
Post a Comment