Monday, February 17, 2014

“KIKWETE AMELIINGIZA TAIFA VITANI”….DK. SLA

SLAA
KAULI aliyopata kuitoa Waziri Mkuu Mizengo Pinda bungeni kuwataka polisi wawapige wapinzani, na kauli ya juzi ya Rais Jakaya Kikwete kuwaagiza wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wajibu mapigo pale wanaposhambuliwa na wapinzani, imeelezwa kuliingia taifa vitani.
Akifungua kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM taifa mjini Dodoma, Rais Kikwete ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho taifa, alisema bila kumung’unya maneno akiwataka Wana-CCM kuacha unyonge na kujibu mashambulizi pale wapinzani wanapoendesha siasa za vurugu.
Waziri Mkuu Pinda katika kipindi cha Maswali na Majibu bungeni aliwahi kutoa kauli ya kuwataka polisi wawapige wafuasi wa CHADEMA kwa vile walikuwa wakiendesha maandamano katika sehemu mbalimbali nchini, ambayo Serikali ya CCM ilitafsiri kama vurugu.
Pinda ambaye hivi sasa amefunguliwa kesi mahakamani ya kuvunja katiba kutokana na kauli hiyo, alisema serikali imechoka na haina njia nyingine zaidi ya kuwataka polisi wawapige wapinzani.
Wakitoa maoni yao kuhusu msimamo wa Rais Kikwete, baadhi ya wanazuoni, viongozi wa siasa wameeleza kushangazwa na kauli ya kiongozi huyo mkuu wa nchi kwani ameliingiza taifa vitani.
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amesema kauli ya Rais Kikwete inatisha, inashangaza na haikupaswa kutolewa na kiongozi mkuu wa nchi.
Alisema kauli yoyote inayotolewa na rais pasipo kujali yupo sehemu gani ni amri kwa walio chini yake, na kwamba kinachofuata ni utekelezaji.
“Waswahili wanasema ukishangaa ya Musa utaona ya Firauni. Hivi karibuni tulishangaa kauli ya Pinda kutaka polisi wawapige tu wapinzani, leo rais naye anawataka CCM waache unyonge, wajibu mapigo. Hii ni hatari sana,” alisema Dk. Slaa.
“Kwa maoni yetu, CHADEMA tunasema Rais Kikwete ameliingiza taifa vitani, amefungua milango ya uvunjifu wa amani, kinachofuata ni umwagaji damu.”
Dk. Slaa aliongeza kwa kusema kuwa anatilia shaka uwezo wa Rais Kikwete katika kuchambua taarifa
anazofikishiwa mezani na wasaidizi wake, ambazo safari hii zimemfanya aamini wanaoanzisha vurugu katika uchaguzi ni wapinzani.
Alisema licha ya Tume ya Jaji Amir Manento na ile ya Haki za Binadamu kulitaja Jeshi la Polisi na CCM kuwa chanzo cha vurugu zinazosababisha mauaji ya watu nchini, Rais Kikwete ameziba masikio na kuwarushia tuhuma hizo wapinzani.
“Watu wameuawa Nyololo na Arusha, ripoti ya Haki za Binadamu anayo ofisini kwake ameifungia na kisha ametoa zawadi ya kuwapandisha vyeo wale waliosababisha mauaji hayo, leo anathubutu vipi kusema wapinzani ndio chanzo cha vurugu?” alisema na kuhoji Dk. Slaa.
Alisisitiza kuwa licha ya Rais Kikwete kuwasingizia wapinzani kuwa chanzo cha fujo, bado ameshindwa kuunda tume huru ya kimahakama ili kuujua ukweli wa matukio hayo.
Alisema kimsingi CHADEMA haitakubali damu ya Mtanzania hata mmoja imwagike kwa sababu ya kupata madaraka, na kwamba agizo la Rais Kikwete linavilazimisha vyama vya upinzani kuwaandaa vijana wao ili kujilinda.
“Hivi kama na sisi tutaamua kuwaambia vijana wetu wajilinde, na katika hali hii ya kunyanyaswa na kuonewa na hao CCM kwa kushirikiana na vyombo vya dola, unadhani nchi itabaki salama?” alihoji Dk Slaa.
Mwenyekiti wa Chama Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amemsikitikia Rais Kikwete kwa kupoteza uelekeo wa kulinda amani ya nchi.
Alisema ameshtushwa na kauli hiyo aliyoieleza kuwa imekosa uvumilivu wa kisiasa, huku akiainisha kuwa chanzo cha vurugu katika sehemu mbalimbali nchini ni CCM kwa kushirikiana na vyombo vya dola.
Alisema alitegemea Rais Kikwete ahimize Watanzania kutii sheria bila shuruti badala ya kuonyesha dalili za wazi kuwa hakuna haja ya kutii sheria, na hata vyombo vinavyotafsiri sheria hiyo.
“CCM ndio waanzilishi wa vurugu zote nchini, na kama mwenyekiti wao ametoa kauli hiyo, unategemea nini kitatokea ikiwa yeye ndiye amiri jeshi mkuu?” alihoji Lipumba.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, kwa upande wake alisema kauli ya Rais Kikwete itamfanya abebe dhamana juu ya jambo lolote la uvunjifu wa amani litakalotokea kuanzia sasa.
Alisema ni hivi karibuni taifa liliingia katika maridhiano ya kuandika katiba mpya kwa ajili ya Watanzania, hivyo Rais Kikwete hakupaswa kutoa kauli hiyo wakati huu.
“Hii kauli haina viashiria vizuri kwa taifa, ni vema aje hadharani atuambie alikusudia nini, vinginevyo atabeba dhamana ya jambo lolote litakalojitokeza,” alisema.
Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ambaye ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na jamii, Bashiru Ally, alisema Watanzania wategemee visa vingi wakati huu wa kuelekea uchaguzi wa 2015.
Alisema nchi inaweza kuingia kwenye machafuko ambayo hayajawahi kutokea
kutokana na kauli za wanasiasa, zinazolenga kuwanufaisha wao binafsi badala ya maslahi ya taifa.
Aliongeza kuwa kitendo cha Mwenyekiti wa CCM kuwaagiza wafuasi wake wasiwe wanyonge na wajibu mapigo, siyo suluhisho la tatizo bali ni kuongeza tatizo.
Alisema NEC ya CCM badala ya kukaa na kuamua kupambana, wangetafuta jibu juu ya kiini cha mapambano hayo yanayodaiwa kutokea katika jamii.
“Mwenyekiti amekuja na majibu mepesi katika maswali magumu, na mimi nasema kuchoka uvumilivu si jawabu la tatizo, wajitokeze hadharani kutibu chanzo,” alisema Bashiru.
Alisema rais kuruhusu hali hiyo ni kutangaza vita ya wenyewe kwa
wenyewe kwa kuwa kauli yake ni amri kwa walio chini yake, na kwamba wananchi watakapokataa kunyanyaswa, madhara yake yatakuwa makubwa kwa jamii nzima.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu, alipoulizwa kama kauli ya rais inaashiria Jeshi la Polisi limeshindwa kutekeleza wajibu wake wa kuwalinda Watanzania na pia kama si uchochezi wa wazi, alisema hajapata taarifa hizo wala kusikia, na kwamba atafanyia kazi ajue kama alichoelezwa kimetamkwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa.
“Mimi ndiyo kwanza ninasikia kutoka kwako, wewe ndiyo unaniambia, ngoja nifuatilie nijue kama kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa CCM,” alisema IGP Mangu.
Akifungua mkutano wa NEC ya CCM juzi mjini Dodoma, Rais Kikwete aliwataka wanachama wa chama hicho kuacha unyonge kwani uvumilivu waliokuwa nao umefika kikomo chake.
Alisema chama hicho kinaingia kwenye uchaguzi mdogo katika Jimbo la Kalenga mkoani Iringa, kinashindana na vyama vingine ambavyo alisema ni wagomvi, maana kwao ugomvi ndiyo sehemu ya mwongozo wa kufanya kazi ya siasa.
“Tulizungumza nalo hilo kwenye Kamati Kuu, tulikubaliana kuacha unyonge. Ndiyo, kwenye Kamati Kuu tumekubaliana, tumesema jamani watu wote waende wakaseme tumekubaliana kuacha unyonge,” alisema huku akicheka na kupigiwa makofi na wajumbe wa NEC.
Rais Kikwete ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu, alitolea mfano wa tukio lilitokea Kahama mkoani Shinyanga, ambapo kijana mmoja alitolewa macho kwa bisibisi, na tukio la Igunga ambapo kijana mmoja alimwagiwa tindikali katika uchaguzi mdogo wa jimbo hilo.
“Acheni unyonge na hata katika taarifa ya habari leo (jana) mtoe hivyo hivyo. Na muache habari zote mseme hii tu (waandishi wa habari). Uvumilivu una ukomo wake,” alisema huku wajumbe wakiendelea kumpigia makofi.
“Nalisema kwa sababu yanayotokea yanasikitisha sana. Pale Igunga kijana yule wamemmwagia tindikali, pale Kahama kijana ametolewa macho kwa bisibisi,” alisema.
Uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Kalenga lililopo mkoani Iringa unatarajiwa kufanyika Machi 16, mwaka huu, huku tayari vyama vya CCM na CHADEMA vikiwa vimetaja wagombea wao.
Chanzo Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment