Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP)
Liberatus Sabas akitoa elimu ya Ulinzi Shirikishi kwa viongozi na
wananchi wa Tarafa ya Endabashi iliyopo wilayani Karatu. (Picha na
Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha) Diwani
wa kata ya Buger Bw. Emmanuel Tlaqho akitoa shukrani zake kwa Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Arusha (SACP) Liberatus Sabas mara baada ya kueleza
uanzishaji wa kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto katika eneo hilo.
(Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha) Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP)
Liberatus Sabas katikati akiwa katika picha ya pamoja na viongozi na
baadhi ya wananchi wa Tarafa ya Endabashi mara baada ya kumaliza kutoa
elimu ya ulinzi shirikishi kwa wakazi hao. (Picha na Rashid Nchimbi wa
Jeshi la Polisi Arusha)
…………………………………………………………………………………………………………..
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Wananchi
wa Tarafa ya Endabashi iliyopo wilayani Karatu wamefurahishwa na
utaratibu mpya wa jeshi la Polisi wa kupeleka askari 15 kila Tarafa kwa
lengo la kuimarisha ulinzi katika maeneo yao. Akimshukuru Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Arusha, kwa niaba ya wananchi hao Diwani wa kata ya Buger
Bw. Emmanuel Tlaqho, alisema kwamba mbali na mpango huo pia wamepokea
kwa mikono miwili uanzishaji wa Dawati la Jinsia na Watoto.
Bw.
Tlaqho alisema kwamba Dawati hilo litasadia katika mambo mengi ya
kijamii ikiwa ni pamoja na kutatua migogoro ya ndoa na utelekezwaji wa
familia. Alisema pamoja na kuwepo kwa Dawati hilo pia viongozi wa mtaa
wa maeneo hayo wanatakiwa kushirikiana na Jeshi la Polisi katika
utekelezaji wa majukumu yake ikiwa ni pamoja na kuwaasa wanandoa ili
waishi kwa amani ndani ya familia zao pia kutotumikisha watoto pamoja na
kutowanyanyasa.
Naye
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi
(SACP) Liberatus Sabas akizungumza na viongozi na wananchi wa maeneo ya
Tarafa hiyo ambayo ina jumla ya vijiji 16 na wakazi wapatao 68,339,
alisema kwamba mpango huo wa kupeleka askari 15 kila Tarafa una nia ya
kuliweka Jeshi la Polisi karibu na wananchi ili waweze kushirikiana
katika utatuzi wa matatizo ya kiulinzi na kiusalama kabla hayajafika kwa
Mkuu wa Polisi wa wilaya.
Kamanda
Sabas aliongeza kwa kusema kwamba, mbali na askari hao kuimarisha
ulinzi katika maeneo hayo pia watakuwa wanatoa elimu ya Polisi Jamii kwa
askari wa vikundi vya ulinzi shirikishi ili wajue namna ya utendaji wa
kazi za ulinzi ikiwa ni pamoja na ukamataji salama na pia kutoa elimu
kwa wananchi kupitia mikutano mbalimbali ili waweze kujua haki zao na
wajibu wao katika suala zima la ulinzi.
Kamanda
Sabas aliwasisitizia wakazi wa Tarafa hiyo wawe wanatumia mbinu za
Ulinzi Jirani katika nyumba zao. Alisema suala la ulinzi ni la kila
mmoja na haliihitaji kusubiri kudra ya M/mungu kwani uwezo wa kuzuia
uhalifu upo ndani yao.
Akimalizia
kutoa elimu hiyo kwa wakazi hao, Kamanda Sabas aliwaambia katika suala
la ulinzi itikadi za kisiasa na udini hazina nafasi kwani mhalifu
anapovamia eneo lolote hamuulizi mtu kwamba ni wa Chama gani au Dini
gani bali yeye anatekeleza kile alichokikusudia.
Kwa
upande wake mwananchi mmoja aliyejitambulisha kwa jina la John Bula
alisema kwamba, inaonyesha dhahiri kwa sasa jeshi la Polisi limeamua
kushirikiana na wananchi kwani katika maisha yake hayawahi kuongea na
Kamanda wa Polisi wa Mkoa ana kwa ana mbali ya kumuona kwenye runinga au
akiwa katika msafara wa Viongozi wa kitaifa lakini kupitia kikao hicho
ameweza kuongea naye.
Bw.
Bula alisema kutokana na hamasa iliyotolewa na Kamanda Sabas yeye kwa
kushirikiana na wananchi wenzake watakuwa bega kwa bega na askari hao
waliopo tarafani hapo ambao wanaongozwa na Mkaguzi Msaidizi wa Polisi
Robert Majenga.
Mpaka
hivi sasa katika Mkoa wa Arusha tayari Kamanda Sabas amekwisha toa
elimu juu ya ulinzi shirikishi kwa wananchi wa Tarafa mbalimbali za
wilaya nne huku bado akisubiri kumalizia wilaya mbili ambazo ni
Ngorongoro na Longido.
No comments:
Post a Comment