1.0 UTANGULIZI
Mamlaka ya Mawasiliano imepokea matokeo ya
tathmini ya zoezi la uhamaji toka mfumo wa utangazaji wa analojia kwenda
kidijiti. Zoezi hili lilifanyika kwenye miji saba kama ilivyotajwa
kwenye taarifa iliyotolewa na wataalamu wa Chuo kikuu cha Dar e salaam
waliofanya tathmini ya Uzimaji wa Mitambo ya Analojia katika Awamu ya
Kwanza.Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)
ilifanya kamisheni kwa Chuo Kikuu cha Dar es salaam kufanya tathmini ya
uzimaji wa Mitambo ya Analojia katika Awamu ya Kwanza, ikitambua kuwa
Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam kuna wataalamu wenye uzoefu mkubwa wa
kufanya tathmini za aina mbalimbali, na kwamba uzoefu huo utasaidia sana
kuhakikisha kuwa tunapata taarifa ya uhakika itakayotuwezesha kuboresha
zoezi hili kwenye awamu inayofuata.Nachukua
nafasi hii kuwapongeza wataalamu waliohusika katika tathmini hii kwa
weledi wao kwenye kazi hii muhimu kwa taifa letu kulingana na matokeo
yaliyowasilishwa kitaalamu mbele yenu waandishi wa habari leo hii.Tanzania
ni nchi ya kwanza kuzima mtambo ya analojia Barani Afrika. Uamuzi wa
kufanya hivyo, na matokeo yake, umeiletea sifa kubwa nchi yetu kwa jinsi
ambavyo Tanzania ilijipanga na kutekeleza maazimio yaliyofikiwa
kimataifa kwa wakati na weledi mkubwa. Hii imeonyesha wazi jinsi
Serikali ilivyoweza kushirikiana na taasissi zake pamoja na wadau wote
katika kutimiza azma hii iliyoafikiwa kimataifa tangu 2006.Zoezi
la uzimaji mitambo kwa awamu ya kwanza iliyoanza taree 31 disemba 2013
halikuwa rahisi kama wengi wetu tunavyoweza kufikiria, kwani liligusa
nyanja nyingi zikiwemo za kijamii, kibiashara, kiufundi na Kisiasa.
Mamlaka kama mdhibiti wa sekta ya Mawasiliano, ilibidi kuzingatia
matakwa ya nyanja zote na wadau mbalimbali bila kuathiri utoaji wa
habari nchini. Inakadiriwa kuwa mpaka kumaliza zoezi hili, mitambo ya
kurushia matangazo kwa mfumo wa analojia isiyopungua 60 itakuwa
imezimwa. Hali hii imefanya Tanzania kuwa nchi ya pekee na kuifanya nchi
yetu kuwa kituo cha mafunzo kwa nchi nyingi ambazo sasa zimekuwa
zikifika kujifunza hapa nchini.
Uamuzi wa kufanya mkutano wa nchi za SADC na ule
wa nchii za Jumuiya ya Madola kuhusu Mfumo mpya wa utangazaji wa
kidijiti kwa sekta ya utangazaji hapa nchini hivi karibuni, ni matokeo
ya mafanikio makubwa tuliyo yapata kwenye zoezi hili lililoendeshwa
kitaalamu na Serekali yetu kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
(TCRA).
2.0 UPELEKAJI WA MKONGO WA TAIFA KWENYE VITUO VYA KURUSHIA
MATANGAZO
Mamlaka ya Mawasiliano kwa kushirikiana na
Wizara na Kampuni ya Simu ya TTCL tuko kwenye mchakato wa kuhakikisha
kuwa vituo vyote vya kurushia matangazo vinafikiwa na mkongo wa Taifa
(Optic fiber cable).
Madhumuni ya jitihada hizi, ni kuona kuwa mbali
na huduma ya msingi ya kurusha matangazo ya televisheni, vituo vya
utangazaji vinatoa huduma za ziada zipatikanazo kwenye mfumo wa
kidijiti. Kwa lugha ya kitaalam ni “interactive services”. Napenda
kuchukua nafasi hii kuvitaka vituo vya utangazaji vyote nchini kuwa
wabunifu na kutumia fursa zilizopo kwenye teknolojia hii ya kidijiti ili
wananchi waweze kuona tofauti kubwa kati ya mfumo wa zamani wa analojia
na huu mpya wa kidijiti.
3.0 UZIMAJI MITAMBO YA ANALOJIA AWAMU YA PILI
Baada ya kupokea matokeo ya tathmini Awamu ya
Kwanza, Mamlaka ya Mawasiliano inajipanga kuzima mitambo kwa awamu ya
pili na ya mwisho. Katika awamu hii, inategemewa miji 12 itahusika na
uzimaji wa mitambo ya analoja. Lakini kama maafikiano yalivyofanyika
awali, uzimaji utafanyika tu pale ambapo huduma za utangazaji wa
kidijiti umefika. Vigezo vyote vitano tulivyokubaliana na wadau
vitahakikishwa kuwa vinatimizwa kabla ya kuzima mitambo hiyo.
Ni matarajio ya Mamlaka kuwa wasimikaji wa
mitambo ya kidijiti (Multiplex Operators) wataendelea kwa kasi ufungaji
wa mitambo hiyo hasa kwenye maeneo ambayo mfumo wa analojia unatumika.
Mpaka sasa miji mingine 7 inapata huduma ya matangazo ya kidijiti nayo
ni Morogoro, Singida, Tabora, Musoma, Kigoma, Bukoba na Kahama. Mchakato
wa kufunga mitambo ya kidijiti kwenye miji iliyobaki inaendelea vizuri.
Tunatarajia kuwa vituo vya utangazaji vitatoa ushirikiano mkubwa kama
ule tulioupata kwenye awamu ya kwanza.
Mamlaka imeyachukua mapendekezo yote
yaliyotolewa kwenye ripoti hii na tunaahidi kuwa tutayafanyia kazi. Yale
yaliyo nje ya uwezo wetu tutayafikisha mahali panapohusika kwa
utekelezaji zaidi.
Mwisho, napenda kuwafahamisha kuwa Mamlaka
imependekeza rasimu ya ratiba ya uzimaji mitambo awamu ya pili na ya
mwisho itakayotangazwa na Waziri mwenye dhamana ya sekta ya Mawasiliano
hivi karibuni.
Katika mapendekezo ya Mamlaka, tunakusudia
kuanza awamu ya pili katika miji ya Singida na Tabora mnamo mwishoni wa
mwezi Machi 2014. Miji mingine katika awamu ya pili itakuwa Musoma,
Bukoba, Morogoro, Kahama, Iringa, Songea na Lindi. Awamu ya pili
inategemewa kukamilika mwishoni mwa mwezi Oktoba 2014.
Nia ya Mamlaka ni kuona zoezi hili la uhamaji
kutoka mfumo wa utangazaji wa analojia kwenda mfumo wa kidijiti
linakamilka katika nchi yetu kabla ya kufikia ukomo wa matangazo ya
analojia kama ilivyoelekezwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia Mawasiliano Duniani (ITU) siku ya tarehe 17 Juni 2015.
Imetolewa na:
MKURUGENZI MKUU
MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA
19 February 2014
No comments:
Post a Comment