Nape Moses Nnauye Katibuwa Itikadi, Siasa na Uenezi akizungumza na waandishi wa habari leo mchana katika makao makuu ya CCM Lumumba ofisi ndogo ya chama jijini Dar es salaam kuhusu maamuzi ya vikao vya chama vilivyomalizika mjinDaodoma hivi karibuni.
…………………………………………………………………………………..
Kati ya tarehe 13/02/2014 na tarehe 18/02/2014 kumekuwa na
mfululizo wa vikao kadhaa vya Chama kitaifa vilivyoshughulikia suala la
maadili ndani ya Chama.
Vikao hivyo ni pamoja na Kamati Ndogo ya Udhibiti tarehe
13-14/02/2014, Tume ya Udhibiti na Nidhamu 18/02/2014 na Kamati Kuu
tarehe 18/02/2013.
Waliohojiwa katika mfululizo wa vikao hivi ni wafuatao:-
1. Ndg. Frederick Sumaye
2. Ndugu Edward Lowasa
3. Ndugu Bernard Membe
4. Ndugu Stephen Wassira
5. Ndugu January Makamba
6. Ndugu William Ngeleja
Baada ya kuwahoji ilithibitika
kuwa baadhi ya tuhuma dhidi yao ni za kweli na hivyo kupendekeza
adhabu. Mapendekezo hayo yalipelekwa kwenye Tume ya Udhibiti na Nidhamu
na hatimaye Kamati Kuu ya CCM ambayo ilitoa adhabu kwa wahusika.
Kwa ujumla waliohojiwa wamethibitika kuwa na makosa yafuatayo:-
1. Walithibitika kuanza kampeni
za kutafuta kuteuliwa kugombea Urais kabla ya wakati kinyume na Kanuni
za Uongozi na Maadili za CCM Toleo la Februari 2010, Ibara 6(7)(i).
2. Wamethibitika kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani
ya Chama na baadhi yao kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya
jamii. Kosa hili nalo ni kwa mujibu wa Kanuni za Uongozi na Maadili za
CCM Toleo la Februari 2010, Ibara kadhaa za kanuni hizo.
Kamati Kuu baada ya kuthibitisha makosa hayo imewapa watu wote
sita waliohojiwa adhabu ya ONYO KALI na kuwataka wajiepushe na vitendo
vinavyokiuka maadili na iwapo wataendelea na vitendo hivyo Chama
kitawachukulia hatua kali zaidi.
Tafsiri ya adhabu ya ONYO KALI kwa mujibu wa Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM Toleo la Februari 2010, Ibara ya 8(ii) (b) ni:-
“Mwanachama aliyepewa adhabu ya ONYO KALI atakuwa katika hali ya
kuchunguzwa kwa muda usiopungua miezi 12, ili kumsaidia katika jitihada
zake za kujirekebisha.”
Kamati Kuu imeitaka pia Kamati Ndogo ya Udhibiti kuwachunguza na
kuchukua hatua kwa wote waliohusika kwa namna moja au nyingine
(mawakala na wapambe) kufanyika kwa vitendo hivyo vilivyovunja Kanuni za
Chama.
Aidha, Kamati Kuu imewaonya vikali Viongozi na Watendaji wa
Chama na kuwataka kujiepusha kujihusisha na matendo ya wanawania Urais
yanayovunja na kukiuka maadili ya Chama, wametakiwa kuzingatia Kanuni na
taratibu za Chama.
Imetolewa na:-
Nape Moses Nnauye, KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA, ITIKADI NA UENEZI, 18/02/2014
Nape Moses Nnauye, KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA, ITIKADI NA UENEZI, 18/02/2014
No comments:
Post a Comment