WAKATI
mjadala wa kihistoria wa kuunda Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, ukiwa katika hatua ya kupata kanuni za Bunge Maalumu la
Katiba, baadhi ya wajumbe wameamua kuelekeza nguvu kudai posho nono.
Wajumbe
hao wanapinga posho ya sasa ya Sh 300,000 kwa siku, ambayo kwa wananchi
wa kawaida inaonekana ni kubwa, lakini vielelezo vyao ni taarifa,
kwamba wajumbe ambao wanatoka Baraza la Wawakilishi, wanalipwa zaidi ya
hapo.
Mbali
na hoja hiyo ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, ambayo sasa wajumbe
ambao ni wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, wanafikiria kumbana
Spika Anne Makinda, ili nao waongezwe posho kama wenzao wa Zanzibar,
hoja nyingine imetajwa kuwa ni hadhi ya wabunge kwamba haifanani na Sh
300,000.
Aliyeanzisha
hoja hiyo jana ni Richard Ndassa, Mbunge wa Sumve, ambaye mbali na
kutaka nyongeza ya posho, alipinga utaratibu wa kusaini asubuhi na jioni
kwa ajili ya posho zinazotolewa ‘rejareja’, akipendekeza waaminiwe na
walipwe fedha nyingi kwa mkupuo.
Mjumbe
mwingine, Suleiman Nchambi, alimwunga mkono Ndassa, lakini akahoji
iweje wajumbe wa Tume ya Kurekebisha Katiba walipwe posho kubwa nao
walipwe kidogo.
Mezani kwa Serikali
Kutokana
na hoja hizo, Mwenyekiti wa muda wa Bunge, Pandu Ameir Kificho, alisema
suala hilo linachukuliwa kwa umuhimu na watazungumza na Serikali
liamuliwe baadaye.
“Kuhusu
masuala ya posho, kama nilivyosema tunalichukua ili tuangalie uwezekano
wa kuzungumza na Serikali, hili tutaamua hapo baadaye,” alisema
Kificho.
Tume
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Bunge, Ndassa
alisema wajumbe wa Tume walikuwa wakilipwa Sh 500,000 kwa siku huku
madereva wakilipwa Sh 220,000.
“Mimi
ninayehangaika kuanzia asubuhi na mimi nalipwa Sh 220,000? Mimi mjumbe
wa Bunge Maalumu la Katiba na dereva wa Tume ni sawa?” Alihoji Ndassa.
Katika
Sh 300,000 kwa siku, Sh 80,000 ndiyo posho ya kujikimu ambayo wajumbe
wa Bunge la Katiba watapewa kila siku, iwe amefanya kazi au la, na Sh
220,000 ni posho ya kazi, ambayo itatolewa kwa waliofanya kazi tu.
Hadhi
ya Mbunge “Mimi kwenye hizi laki tatu (Sh 300,000) zangu zote, ni
pamoja na dereva wangu, simu, chakula, mafuta, lakini pia unamtaka
mbunge eti lazima asaini kwanza!” Alionesha mshangao.
Bila
kupendekeza kiwango cha kulipwa, Ndassa alitoa mchanganuo wa matumizi
ya mbunge, akisema hoteli ya hadhi yake ni Sh 70,000 kwa usiku mmoja.
Mbali
na gharama hiyo ya malazi, alisema gharama za chakula, mafuta ya gari,
dereva na msaada atakaotakiwa kutoa kwa watu mbalimbali Sh 80,000
haitoshi.
“Hoja
yangu ya msingi, ni kwamba Serikali ijaribu kuangalia suala hili kwa
upana, tukiliacha hivi hivi linaweza kuleta tatizo,” alisema Ndassa.
Kususa
Ndassa
alisema wabunge wengine ni wafanyabiashara ambao hawawezi kukubali
kukaa bungeni kwa muda wote wakilipwa posho ya Sh 300,000.
Alipohojiwa
anatarajia mtazamo gani kutoka kwa wananchi wanaoishi kwa kipato cha
chini ya dola moja kwa siku (Sh 1,600), huku yeye akikataa Sh 300,000
kwa siku, Ndassa alisema: “Ukiweka matarajio ya jamii itasemaje, huwezi
kufanya kazi. Maswali kama hayo huwezi kuyakwepa, binadamu hamwezi
kulingana nyote duniani, hata vidole viko tofauti.”
Nchambi
alisema kwa upande wao, wabunge hawana tatizo isipokuwa anatetea
wajumbe wengine ambao hawalipwi kiinua mgongo wala mshahara.
“Mbunge
anatakiwa alale kwenye hoteli ya angalau Sh 70,000. Hata wananchi
wanatakiwa waelewe kwamba wabunge wamekuja kufanyia kazi Katiba ambayo
ndiyo msingi wao,” alisema Nchambi.
Ubaguzi
Suala
lingine lililoibuliwa na Ndassa nje ya ukumbi, ni kuhusu tofauti ya
kiasi cha posho kwa alichosema wajumbe wa Baraza la Wawakilishi,
wameongezwa Zanzibar wakati wengine wakipokea Sh 300,000.
Bila
kutaja kiasi kilichoongezwa, Ndassa alisema:“Lakini wenzetu Wazanzibari
wameongezwa na Baraza la Wawakilishi, wote ni wajumbe wa Bunge
hilohilo… lazima kutakuwa na mgawanyiko. Na sisi tukisema hawa wabunge
wamekwenda kwao wameongezwa na sisi tumwambie Makinda atuongeze, hawa
makundi maalumu watakwenda kuongezwa wapi?
“Kwa
kufanya hivyo umeshaweka mgawanyiko inatakiwa tuwe kitu kimoja, kama ni
Sh 20 wote tupewe Sh 20, kama ni Sh 800 wote tuwe sawa,” alisema
Ndassa.
Mwandishi
wa habari hizi hakufanikiwa kumpata Katibu wa Baraza la Wawakilishi,
Yahya Khamis Hamad kufafanua hilo kutokana na kuwa kwenye kikao.
Lakini
taarifa kutoka kwa baadhi ya watendaji wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar (SMZ), zilithibitisha kwamba wawakilishi waliomba waongezwe Sh
500,000 lakini hawakupewa zote; wamepewa chini ya hapo.
“Si
kweli (hawapokei Sh 420,000) lakini waliomba Sh 500,000 ila hawakupewa
hizo, wamepewa chini ya hapo,” alisema mtoa habari ambaye hakusema ni
kiasi walichoongezwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Utaratibu
Kwa
mujibu wa Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah, wabunge hao
wameshapewa posho ya kujikimu ya Sh 80,000 kwa siku kuanzia Februari 16
hadi 28.
Aliongeza
kuwa posho maalumu ya kazi ya Sh 220,000 kwa siku, ambayo hupigiwa
hesabu kutokana na ushiriki wa mjumbe kusaini mahudhurio kila siku
asubuhi na jioni, itakuwa ikiingizwa kwenye akaunti za wajumbe kila
baada ya wiki moja ya kazi.