Wednesday, February 26, 2014

Wananchi wataka Posho ya wabunge wa Bunge la Katiba ipunguzwe kutoka 300,000 hadi 170,000


Bunge la Katiba
WAKAZI wa wilaya za Tarime na Rorya mkoani Mara, wameshauri kupunguzwa kwa posho za wajumbe wa Bunge maalumu la Katiba kutoka Sh 300,000 hadi Sh 170,000 ambazo walisema ni za kawaida kwa vikao vya Bunge.
Wamewaomba pia wajumbe hao ambao wamekwenda kuwawakilisha wenzao kuweka maslahi ya Taifa mbele na kuacha tamaa za kujipatia fedha nyingi ambazo ni kodi za wananchi.
Waliotoa ushauri huo ni Sigirya Mwita ambaye ni Mwenyekiti wa CCM wa Kata ya Pemba, Peter Mwera ambaye ni Diwani wa CCM wa Kata ya Mriba na Nyangoko Paulo ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji Sirari kupitia Chama cha Chadema.
Wengine ni wananchi wa kawaida Otieno Igogo, Matiko Majani, Elizabeth Mseti, Ores Lameck, Kansela Sereria, Maria Bhoke na Gimase Marwa.
Viongozi na wananchi hao walisema hawakubaliani na maombi ya wabunge hao ya kuomba serikali kuwaongezea posho na badala yake wapunguziwe kutoka Sh 300,000 za sasa hadi Sh 170, 000 ambazo ndizo zinazokubalika kisheria kwa vikao.
“Katiba hii wanayoijadili ni ya Watanzania wote hata wao wamo na familia zao. Hawakupendekezwa kwenda kujitafutia mitaji na kutaka kuhujumu uchumi wa nchi. Kuna baadhi yao humo hawapati au kuzalisha hata Sh 100,000 kwa siku kwao.
“Kisingizio kuwa ni wajumbe wa Bunge maalumu la Katiba hakina mashiko.Tunaomba Serikali kutowaongeza posho hizo badala yake zipunguzwe kwani fedha hizo ni za wananchi ambazo zingine hupelekwa katika kutekeleza miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa madarasa, nyumba za walimu, barabara, kuchimba visima vya maji na kuwasomesha wanafunzi waliokwama kuendelea na masomo,” walisema kwa nyakati tofauti.

No comments:

Post a Comment