Wednesday, February 26, 2014

MAGARI YATEKWA ABIRIA WAPEWA KICHAPO BARABARA YA MBEYA - NJOMBE

WATU wasiofahamika majina wala makazi yao, juzi walifunga Barabara Kuu ya Mbeya-Njombe, Wilaya ya Mbarali, mkoani Mbeya kwa kuweka mawe, magogo, kuteka magari na kujeruhi abiria waliokuwa katika magari hayo.

 Akizungumza na waandishi wa habari mjini Mbeya jana, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani humo, Robert Mayala, alisema tukio hilo lilitokea saa 1:30 usiku, Kijiji cha Machimbo, Kata ya Rujewa.

Alisema watu hao walikuwa na silaha za jadi kama mapanga, rungu, mawe na fimbo ambapo katika tukio hilo, baadhi ya abiria walijeruhiwa na kuporwa vitu mbalimbali.

Vitu hivyo ni pamoja na pesa taslimu, simu za mkononi na mikoba ambayo thamani yake wala idadi haijafahamika.
 
"Hawa watu waliwashambulia baadhi ya abiria kwa kuwapiga sehemu mbalimbali za miili yao kwa kutumia silaha ambazo walikuwa nazo, kufanya uharibifu katika baadhi ya magari kwa kuvunja vioo," alisema Kamanda Mayala.

Aliongeza kuwa, katika tukio hilo Bw. Mashaka Abdallah ambaye ni dereva, alijeruhiwa vibaya na kulazwa Hospitali ya Serikali wilayani Mbarali na hali yake inaendelea vizuri; watu wengine wawili walipatiwa matibabu na kuruhusiwa.

Alisema polisi waliokuwa doria eneo la Igawa, Mbeya na Njombe walifika eneo la tukio na magari mengi yakiwemo yanayosafirishwa kwenda nje, yakiwa yamesimamishwa.
 
"Watu hao walipoona gari la polisi walikimbilia vichakani na magari hayo yaliondoka chini ya ulinzi wa polisi kuendelea na safari, watu 10 tunawashikilia kwa mahojiano," alisema.

No comments:

Post a Comment