Sunday, March 23, 2014

MABANDA YANAYOONESHA VIDEO ZA NGONO YAFUTIWA LESENI

Serikali mkoani Pwani  imefuta vibali vya uendeshaji wa mabanda ya kuonyesha  video wilayani Kibaha pamoja na kuanzisha  uchunguzi wa wanafunzi wa shule  msingi wanaojihusisha na vitendo vya ulawiti.
 
Hatua hiyo inachukuliwa  baada ya wanafunzi wa kiume wa shule za msingi wilayani humo kudaiwa kufanya vitendo hivyo vyenye athari kiafya na kitaaluma.
 
Katika hatua nyingine, polisi wilayani humo inawashikilia watu wawili  waliokutwa wakiendesha biashara ya kuonyesha video chafu kwenye mabanda kinyume na sheria.
Toleo la Nipashe la Jumapili iliyopita liliripoti  taarifa za wanafunzi  katika shule tatu zilizopo Mlandizi, wilayani humo wanaojihusisha na  vitendo vya kujaamiana kinyume cha maumbile wenyewe kwa wenyewe, pamoja na watu wengine kutoka nje ya shule hizo wakiwadhalilisha kingono.
 
Taarifa za uhakika zilisema tayari timu maalum imeundwa na uongozi wa mkoa huo kwa ajili ya kuchunguza suala hilo na wajumbe watatembelea  shule zilizotajwa katika  mahojiano na wanafunzi pamoja na walimu.
 
Akizungumza na NIPASHE, Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kibaha, Amedeus Marenge, alisema pamoja na kushikiliwa watuhumiwa hao wawili,  wamefungua jalada  la uchunguzi katika shule mbalimbali wilayani humo kubaini washukiwa.
 
Alisema wanaoshikiliwa siyo kwamba wanahusika moja kwa moja na tuhuma hizo, bali mabanda wanayoyamiliki yanatumiwa kudhalilisha watoto na kuonyesha picha zisizo na maadili.
 
"Kazi ya kuchunguza suala kama hili ni ngumu kwa sababu mambo yote yanafanyika sirini na hakuna  aliyejitokeza kusema ukweli. Uchunguzi wetu unaendelea ….," Alisema Marenge.
 
Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya  aliwataka wananchi hasa wazazi kushirikiana na polisi kwa kutoa taarifa wanapoona mambo yanayowapa mashaka kuhusu mienendo ya watoto wao.
 
HALMASHAURI YAFUTA VIBALI
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kibaha, Tatu Selemani, alisema kuanzia sasa shughuli ya uonyeshaji video kwenye mabanda umepigwa marufuku.
 
Alisema amemuagiza Afisa Utamaduni kufuta vibali pamoja na kuwafuatilia wanaoonyesha picha hizo.
 
"Nimeagiza vibali vyote vifutwe na marufuku kwa kuendesha shughuli hiyo hata kama wana malengo ya kuonyesha soka,"alisema.
 
Uchunguzi wa gazeti hili uliofanywa maeneo hayo ulibaini mabanda mengi ya aina hiyo yamefungwa na kufuli.
 
WANANCHI WAPONGEZA 
Baadhi ya wazazi waliipongeza  serikali kuingilia kati na kuwanusuru wanafunzi ambao walianza kupotoka na kuongeza kuwa kusitishwa uonyeshaji wa picha za video kumewezesha watoto  kuanza kwenda shuleni.
 
"Viongozi wa serikali walikuja hapa Jumatatu na kufunga vibanda hivi jirani na shule za msingi Mtongani na Azimio, tumeanza kuona matokeo mazuri kwani watoto wanakwenda shule na kuhudhuria vipindi ," alisema Hamisi Kondo mkazi wa Mtongani.
Mzazi  mwingine Christopher Steven, aliwapongeza  wanafunzi na walimu walioibua suala hilo kwa kuowaokoa watoto wengi ambao wangeingia katika mazingira hayo hatarishi.
 
"Unajua sisi wazazi tumekuwa na tabia ya kutosikiliza yanayosemwa na walimu, badala yake tunasubiri hadi mambo yawe makubwa ndipo tunashtuka, naamini wanafunzi na walimu wametupa mwanga na nia yao ilikuwa kuokoa watoto wetu, tunashukuru," alisema Steven.
 
Uchunguzi huo ulioibua matukio hayo ulifanywa katika shule za msingi za Mtongani, Azimio na Jamhuri zilizoko  mji mdogo wa Mlandizi na yaliyohusisha wanafunzi wa  darasa la tatu na la nne ambao mara nyingi wanalazimishwa kulawitiwa na wenzao wa madarasa ya juu.
 
Aidha ilidaiwa wanafunzi wengine wanafanyiwa vitendo hivyo na watu wazima wakiwa majumbani kwao na kwenye mabanda yanayoonyesha picha za video nyakati za usiku.
 
Ilielezwa kwamba ndani ya mabanda hayo watoto waliingiliwa na watu wazima  baada ya kuangalia picha za ngono.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment