Michuano
ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaingia
raundi ya 24 kesho (Aprili 5 mwaka huu) kwa mechi mbili ambapo Kagera
Sugar itaikaribisha Simba kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Mechi
nyingine itakuwa kati ya Mbeya City ambayo itakuwa mgeni wa Ashanti
United kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es
Salaam. Ashanti United inayofundishwa na Abdallah Kibaden ipo katika
mkakati wa kukwepa kushuka daraja.
Keshokutwa
(Aprili 6 mwaka huu) kutakuwa na mechi kati ya Coastal na Mgambo
Shooting Stars (Mkwakwani, Tanga), Oljoro JKT na Tanzania Prisons
(Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha), Rhino Rangers na Mtibwa Sugar (Ali
Hassan Mwinyi, Tabora) na Yanga dhidi ya JKT Ruvu (Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam).
Raundi
hiyo itakamilika Aprili 9 mwaka huu kwa mechi kati ya Ruvu Shooting na
Azam itakayochezwa Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
NI MWADUI AU STAND UNITED VPL MSIMU UJAO
Ni ipi
kati ya timu za Mwadui na Stand United, zote za Shinyanga itakayocheza
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao itajulikana kesho (Aprili 5 mwaka
huu) baada ya kundi C kuhitimisha mechi za Ligi Daraja la Kwanza (FDL)
msimu huu.
Mwadui
yenye pointi 28 ndiyo inayoongoza, na itacheza na Polisi Dodoma kwenye
Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma. Nayo Stand United yenye pointi 26
itaikaribisha Toto Africans kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Mechi
nyingine zitakuwa kati ya Pamba na Kanembwa JKT itakayochezwa Uwanja wa
CCM Kirumba jijini Mwanza wakati Polisi Mara na Polisi Tabora
zitakwaruzana kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma.
Timu ambazo tayari zimepanda daraja kutoka FDL kucheza VPL msimu ujao ni Ndanda SC kutoka kundi A na Polisi Morogoro ya kundi B.
21 ZA KUCHEZA RCL ZAJULIKANA
Timu 21
kati ya 27 zitakazocheza Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) kutafuta tiketi
ya kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao tayari zimejulikana.
Timu hizo
ni Abajalo SC (Dar es Salaam), AFC (Arusha), African Sports (Tanga),
Bulyanhulu FC (Shinyanga), Geita Veterans (Geita), JKT Mafinga (Iringa),
JKT Rwamukoma (Mara), Kariakoo SC (Lindi), Kiluvya United (Pwani),
Milambo SC (Tabora) na Mshikamano FC (Dar es Salaam).
Nyingine
ni Mvuvumwa FC (Kigoma), Navy SC (Dar es Salaam), Njombe Mji (Njombe),
Pachoto Shooting Stars (Mtwara), Panone FC (Kilimanjaro), Singida United
(Singida), Tanzanite (Manyara), Town Small Boys (Ruvuma), Ujenzi FC
(Rukwa) na Volcano (Morogoro).
WATANO WAFANYA MTIHANI WA UWAKALA WA WACHEZAJI
Watanzania
watano wamefanya mtihani wa uwakala wa wachezaji wa Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ambao ulifanyika jana (Aprili 3 mwaka
huu) duniani kote.
Watahiniwa
katika mtihani huo ambao ulikuwa na maswali kutoka FIFA na Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) walikuwa Godlisten Anderson, Jesse
Koka, Lutfi Binkleb, Rwechungura Mutahaba na Silla Yalonde.
No comments:
Post a Comment